Confidential Act
Written by Haji Mgogoro
Cc: Simulizi Empire
------------------------
Arusha, Makazi ya Mkuu wa Mkoa. Saa mbili na nusu usiku.
Hali ilikuwa shwari ndani ya makazi ya Mkuu wa mkoa wa Arusha, lakini hatari kubwa ilinyemelea taratibu. Sebuleni aliketi Makame, Mkuu wa mkoa wa Arusha mwenye umri wa miaka 40 huku pembeni yake akiketi Rais wa Tanzania, Laurent Msemo, umri wake haukukatiza miaka hamsini. Wote walitulia tuli wakiendelea kufuatilia taarifa ya habari. Wanausalama wawili wakiume waliovalia suti nyeusi, walisimama kando wakifuatilia kila kitu.
Runinga ilionyesha wananchi kadhaa wakiwa mtaani na mabango yao, wakiandamana kutaka mabadiliko. Mabango hayo yaliandikwa jumbe mbalimbali zilizochochea ari zaidi.
“Mabadiliko ni lazima, tunataka mabadiliko.”
“Hali ni mbaya, achieni fedha.”
“Ajira, ajira, ajira.”
“Mnauza chakula nje ya nchi, sisi tule nini?”
“Hawa watu sijui hata wapoje, yaani wanataka nifanye mabadiliko ndani ya miezi miwili ya madaraka?” Laurent alilalamika, lakini kwa kebehi.
“Hamidi ametuachia msala mzito, Mheshimiwa Rais. Kwanza ni madeni chungu nzima, hali ya kiuchumi ni mbaya, hakuna ajira na vitu ni bei juu.” Makame alijibu baada ya kushushia glasi yake ya maziwa.
“Hamidi ni mshenzi sana, na bado anataka aendelee kunitawala anadhani ataweza? Nimeshaingia madarakani, nitatengeneza serikali yangu kwa maslahi yangu kama ambavyo yeye alifanya kwa maslahi yake.”
“Lakini usisahau nguvu yake, bado anaushawishi kwa viongozi wengi ambao wako kwenye nyadhifa mbalimbali za kiutawala na kiutendaji, wanaweza kukuangusha kiutendaji eidha kwa hila au makusudi.”
Laurent alitabasamu kwa dharau, “Mimi ndiye Rais, Bwana Makame. Yajayo yanafurahisha.” Alijibu kwa kujiamini kisha waliendelea kufuatilia habari.
Wakati huo, mtumishi wa kike aliingia (Zizi) akiwa na sahani mkononi. Mtumishi huyo alivalia suti nyeusi ya suruali, uso wake ulikuwa makini huku macho yake yakicheza kote sebuleni.
Aliweka mezani ile sahani yake yenye vitafunwa, kisha alisogea hadi kwenye dirisha lililopo kando ya sebule. Alitazama kila kona, alipoona hakuna anayemfuatilia, alikunjua pazia kiasi na kuacha kioo cha dirisha kikionekana kisha alivuta kioo taratibu pakapatikana uwazi kidogo. Alipohakikisha kuwa dirisha hilo lipo wazi kiasi, alitoweka haraka pale sebuleni.
Makazi ya Mkuu wa Mkoa yanapakana na Hoteli Zebra HB, mita chache kutoka hapo.
Huko nako shughuli ziliendelea kama kawaida, lakini kwenye ghorofa moja ya juu kabisa, jambo lisilo la kawaida liliendelea.
Chumba kikiwa tulivu, kijana mmoja makini aliweka sawa bunduki yake ya masafa marefu na kufungua dirisha lake. Alipitisha bukundi dirishani, na jicho lake likagota kwenye lenzi. Simu yake iliyopo mezani ilianza kutetemeka na kutoa mlio hafifu, kioo kilionyesha jina la aliepiga ‘Boss’
“Nani anampigia Six sasahivi? Hajui kuwa ni muda wa kazi?” Alijisemea Six pasi na kuyumba toka kwenye windo lake, alipandisha juu bega lake na kulikutanisha na sikio la kulia, alifanikiwa kuchezesha kifaa chake cha mawasiliano kilichopo sikioni.
“Mbona kimya hadi muda huu?” sauti nzito ilisikika kwenye kifaa chake.
“Tulia mkuu, nipo windoni kwa sasa.” Six alijibu kwa ufupi na kurejesha umakini wake kwa kile alichokuwa anakifanya.
Lenzi yake ilimuonyesha vema Rais Laurent akiwa sebuleni na Makame. Taratibu aliachia risasi ya kwanza, kwa mwendo wa haraka, iliacha mdomo wa bunduki kuelekea sebuleni kwa Makame.
Sekunde ileile ambayo risasi imeachiwa, mtumishi mwingine wa kike alikatiza sebuleni kwa lengo la kuhamisha vyombo. FWIP! Mlio hafifu wa risasi ulisikika ukiishia kichwani mwa yule mtumishi.
“Laleni chiniiiii! Tunashambiliwaaa!” Mmoja wa walinzi wa Rais alalipayuka kwa tahadhari, akichomoa bastola yake. Taharuki tayari ilishatokea. Laurent alilala sakafuni pasi na kuchelewa.
“Tambaeni sakafuni, vichwa chini hadi usawa wa mlango.” Mlinzi mwingine aliwajulisha akiwa amejibana kwenye ukuta.
Laurent na Makame walitambaa hadi usawa wa mlango wakiwa kimya na wenye hofu. Walinzi nao walitulia, wakijaribu kusikilizia hali.
“Mheshimiwa Rais usijali, unatoka hapa ukiwa salama kabisa.” Aliongea mlinzi wa kwanza baada ya kupiga hatua moja na kuchungulia kule ambako risasi ilitokea. Baada ya kujihakikishia kuwa kuna usalama, alisimama na kumuinua Rais pamoja na Makame. Walinzi sasa walikuwa nyuma yao, Laurent alifungua mlango, lakini ghafla risasi mbili nyingine ziliachiwa. Looh! Mamake na afisa mmoja walianguka chini huku damu zikitapakaa sakafuni. Haraka sana, mlinzi aliyebaki na Laurent walifanikiwa kutoka nje ambako kulikuwa na askari kadhaa.
“Muwahisheni Rais sehemu salama, haraka harakaa.” Mlinzi aliongea kwa nguvu, askari wale wasiopungua nane waliweka ukuta na kumlinda Rais, wakati huo Chopa ndogo ilitua mkukumkuku, haraka alipandishwa Rais na kupotelea hewani.
Punde tu, vikosi vya usalama vilimiminika kama utitiri, tayari kukabiliana na hali ya hatari.
—--------------
“Boss! Bado yuko hai.” Six aliongea kwa haraka huku anasomba vitu vyake na kuviweka kwenye begi. Ile bunduki yake kubwa ya masafa marefu, aliivuruga na ikawa vipande vipande, vyote vikaishia kwenye begi.
“Hatokuwa na nafasi nyingine, kuna la zaidi?” Sauti ile ile ya mwanzo ilisikika kwenye kifaa chake cha sikioni.
“Mfanyakazi mmoja, afisa usalama mmoja pamoja na Makame wapo chini.”
“Kazi nzuri. Sasa, potea eneo hilo kana kwamba hukuwahi kuwepo.”
“Sawa Boss.” Six alikusanya mkoba wake, akaangalia saa yake kwa haraka, kisha akachukua koti lake na kufunga zipu ya begi. Kwa utulivu, alifungua mlango wa chumba chake na kutoweka kwenye giza la hoteli kana kwamba hakuwahi kuwepo.
—-----------------
Inaendelea...................
Comments
Post a Comment