RIWAYA.
CHAMPION: MOYO USO WOGA.
Imeandikwa na Haji Mgogoro
+255784382101
“SI KILA MWENYE NGUVU HUSHINDA BALI MWENYE MOYO USIO NA WOGA.”
SEHEMU YA 01.
--------------------
Usiku ulifunika jiji la Dar es Salaam kama blanketi jeusi, ukifunika moja ya mtaa wa uswahilini kwa utulivu wa hila. Hali ya hewa ilikuwa ya unyevunyevu na joto, ikiongezwa na msisimko wa watu waliokuwa wakikusanyika kwenye eneo la wazi lililokuwa limetengwa kwa ajili ya burudani ya aina yake. Macho yote yalikuwa yameelekezwa kwenye uwanja wa mapigano, ulioangaziwa na mbalamwezi kali toka angani, ulioandaliwa kwa ajili ya usiku huo wa kusisimua.
Sauti za watu wakicheka, wakibishana, na kusukumana, zilitawala angani, zikisindikiza usiku huu wa kipekee. Kila kona ya mtaa, macho yalikuwa yameelekezwa upande mmoja—uwanja wa mapambano, mahali ambapo damu, jasho, na ujasiri vitakutana.
Katika kona moja ya uwanja, alikuwa amesimama Rocky, mpiganaji chipukizi mwenye umri wa miaka 30. Macho yake yalikuwa makali na mwili uliojengwa vizuri. Alikuwa ameongozana na marafiki zake wawili wa karibu, Hakim na Steve, ambao walikuwa wamefika kumpa moyo, kila mmoja akiwa na hisia mseto za hofu na matumaini.
Huku umati ukiendelea kuongezeka, Franco na Kupa, madalali wajanja wajanja wa mchezo huo, walikuwa wakichochea hisia za watu kwa maneno yao matamu na vitisho vyao. Watu walikuwa wakipiga bet kwa wingi, huku kila mtu akitumaini kwamba mchezaji wake angepata ushindi.
Upande wa pili alisimama Dame, jitu la miraba minne, mwenye uso uliojaa chuki na misuli iliyokaza kama mwamba. Watu walipiga makofi, vigelegele vikapamba usiku, huku wengine wakitoa vitisho vya chini chini, wakishusha pumzi zao kwa hofu ya kile kitakachotokea.
“Na sasa, wananchi wa Dar es Salaaaam!” alipaza sauti Franco kwa mbwembwe, akivutia umakini wa kila mtu. “Karibuni kwenye usiku huu wa kusisimua! Usiku wa mpambano makali! Usiku ambao utaamua hatima ya vijana wawili wenye vipaji!”
“Rocky…Rocky…. Rocky….” Baadhi ya watazamaji walipiga kelele kwa nguvu wakiwa na matumaini makubwa juu ya Mpiganaji wao.
“Dame…Dame…Dame…..” Wengine nao hawakuacha kumtaja Dame. Hakika ilikuwa ni siku iliyosubiriwa kwa hamu kubwa.
Kupa aliongeza kwa kusema, “Katika kona ya bluu, tuna mpiganaji wetu, Rocky! Mwanaume mdogo lakini mwenye moyo wa simba! Na katika kona nyekundu, tuna mfalme wa miraba minne, Dameeee! Je, Rocky ataweza kulishinda jitu hili? Au Dame atathibitisha kwa mara nyingine tena kuwa yeye ndiye mtawala wa mchezo huu?”
Kelele na shangwe ziliibuka tena, hii ilithibitisha kuwa mchezo huu wa masumbwi ndio ambao ulishika hatamu katika mtaa huu wa Kwa Gogo.
Hatimaye, kengele ililia, ikitangaza mwanzo wa raundi ya kwanza. Rocky na Dame walikutana katikati ya uwanja, wakipima nguvu za kila mmoja. Dame alikuwa wa kwanza kushambulia, akitoa ngumi kali ambayo ilimfanya Rocky kupoteza mwelekeo kwa muda. Lakini Rocky alikuwa tayari kwa mashambulizi hayo. Kwa haraka, alijirusha nyuma na kutoa ‘free kick’ kali ambayo ilimfanya Dame kuanguka hadi chini.
Umati ulilipuka kwa shangwe. Hakuna aliyetegemea kwamba kijana mdogo kama Rocky angeweza kumshinda Dame kwa urahisi hivyo. Lakini mchezo ulikuwa bado haujamalizika. Dame aliamua kuonyesha nguvu zake zote, akimshambulia Rocky kwa kasi kubwa.
Raundi ya kwanza iliisha kwa Rocky kupigwa ngumi kali kwenye kidevu. Alianguka chini, lakini aliinuka haraka, akionyesha kuwa hakuwa tayari kukata tamaa. Haraka Franco alipiga kengele kuashiria kumalizika kwa raundi ya kwanza huku Rocky akipoteza. Umati ulikuwa kimya, ukisubiri kuona nini kitatokea katika raundi inayofuata.
—--------------------------------------------------
Usiku ulikuwa unazidi kusonga, gym ilitawaliwa na sauti za pumzi nzito na midundo ya mazoezi ya vijana waliokuwa wakifua misuli chini ya uangalizi wa mkufunzi wao, Gacha Stone. Gacha, mpiganaji hodari aliyekuwa ameweka rekodi ya ushindi na kujikusanyia mikanda kadhaa ya ubingwa, alikuwa akiendelea na mazoezi yake ya kawaida licha ya ushindi wake mkubwa wa siku mbili zilizopita.
Baada ya mazoezi kumalizika, vijana waliondoka mmoja baada ya mwingine, wakimuacha Gacha peke yake katika gym yake tulivu. Alitembea hadi kwenye kabati lake, alifungua, na kutazama medali pamoja na mikanda yake ya ubingwa iliyong'aa. Alirudi kwenye ulingo, akianza tena kufanya mazoezi huku macho yake yakijawa na mng’ao wa ari na mapambano yasiyokoma.
Baada ya muda, aliketi na kupumzika, alikunywa maji huku akitafakari. Ghafla, mlango wa gym ulifunguliwa kwa nguvu, alitokea kijana mtata mwenye macho ya hila, Fabrizio. Alikuwa na uso wa dhihaka, akimkaribia Gacha kwa hatua za kujiamini.
“Kuna nini, kijana?” Gacha aliuliza akiwa bado ametulia.
Fabrizio alitabasamu kwa dharau. “Nimekuja kuonesha nani ni bingwa halisi, na ni wazi kuwa sio wewe.”
Gacha alitabasamu huku anatikisa kichwa. “Ubingwa hauji kwa maneno kijana. Kama unataka pambano, fuata utaratibu, tutapambana rasmi.”
Fabrizio hakujali, bado aliendelea kutamba, “Wewe sio lolote, Gacha. Mikanda yako haina maana. Mimi ndiye bingwa. I'm the Champion”
Gacha alicheka kwa kicheko cha kebehi, kisha alisimama akimtazama Fabrizio moja kwa moja machoni. “Bingwa ni yule anayesimama hadi mwisho. Na bado hujafika huko. Hutokaa kuwa bingwa kamwe, Fabrizio.”
Hapo, Fabrizio hakusubiri tena. Aliamua kuchukua hatua ya ghafla, akirusha ngumi kali kuelekea uso wa Gacha. Gacha alikwepa kwa wepesi, akijaribu kumtuliza Fabrizio kwa busara. Lakini Fabrizio hakuwa na nia ya kuacha, aliendelea kushambulia kwa nguvu zote akirusha ngumi za kasi, mateke ya haraka, na shambulizi zisizo na mpangilio.
Gacha, alikuwa na uzoefu wa miaka mingi, alijaribu kuzuia mashambulizi hayo kwa wepesi na ufundi, lakini alihisi hatari ikiongezeka. Alipoona hali inazidi kuwa mbaya, alijibu kwa mashambulizi makali huku ngumi zake zikiwa kama radi zinazotua kwenye mwili wa Fabrizio. Kila pigo lilikuwa na uzito wa miongo ya mafunzo na vita vilivyopita. Fabrizio alianguka chini, akihema kwa nguvu baada ya mkong’oto mkali toka kwa Gacha.
“Nimekuambia, kijana,” Gacha alisema kwa sauti ya kushusha pumzi, “Wewe ni mpiganaji mzuri lakini huna moyo wa kuwa bingwa. Huwezi kamwe kuwa bingwa. Umejaribu miaka mingi iliyopita lakini ulishindwa.”
Fabrizio alinguruma kwa hasira, akajikusanya tena na kuanzisha mashambulizi upya. Safari hii, alishambulia kwa ghadhabu kali, bila mpangilio. Ngumi na mateke vilishuka kama mvua ya mawe. Gacha, alijaribu kumudu kasi ya mashambulizi hayo, lakini tayari Fabrizio aliazimia lengo baya. Aliendeleza mashambulizi ya kushtukiza na yakikatili. Hatimaye pigo zito lililenga sawasawa na taya ya Gacha, Gacha alianguka chini ya ulingo bila nguvu huku damu zikimtoka.
Fabrizio alihema kwa furaha, alisimama juu ya Gacha, uso wake ukiwa na tabasamu la ushindi. Bila kufikiria mara mbili alimnyonga Gacha kisha alichukua kiberiti na kuchoma moto kabati lililokuwa na medani na mikanda ya ubingwa ya Gacha. Moto ulipokolea, Fabrizio alitoa Markpen kutoka mfukoni mwake, aliinama na kuandika kwenye kifua cha Gacha kwa maandishi makubwa ya kibabe - "CHAMPION."
Alisimama na kutazama kazi yake, Fabrizio alijisikia kama mfalme. “Mimi ndiye bingwa, i'm the Champion.” alijitangaza kwa sauti kubwa, baadaye alitoka nje ya gym na kumuacha Gacha akiwa amelala chini amefariki huku mwili wake ukiwa na alama ya ushindi uliojaa dharau.
—------------------------------------
Raundi ya pili ilianza mara baada ya kengele kupigwa, kelele za mashabiki zilianza tena kwa kasi huku kila mmoja akitaja jina la mpiganaji wake.
Itaendelea……………

Comments
Post a Comment