RIWAYA
CHAMPION: MOYO USOWOGA
Imeandikwa na Haji Mgogoro
+255784382101
SEHEMU YA 02.
Ilipoishia……………
Alisimama na kutazama kazi yake, Fabrizio alijisikia kama mfalme. “Mimi ndiye bingwa, i'm the Champion.” alijitangaza kwa sauti kubwa, baadaye alitoka nje ya gym na kumuacha Gacha akiwa amelala chini amefariki huku mwili wake ukiwa na alama ya ushindi uliojaa dharau.
—------------------------------------
Raundi ya pili ilianza mara baada ya kengele kupigwa, kelele za mashabiki zilianza tena kwa kasi huku kila mmoja akitaja jina la mpiganaji wake.
Endelea………………..
Raundi ya pili ilianza mara baada ya kengele kupigwa, kelele za mashabiki zilianza tena kwa kasi huku kila mmoja akitaja jina la mpiganaji wake.
“Vipi umechukua za kutosha?” Steve alimuuliza Hakim, Hakim ambaye alikuwa anahesabu fedha.
“Za kutosha zaidi ya zile zilizopita, leo tutakula dau ndefu sana. Kila mtu kamwekea Dame kwa kuamini kuwa anashinda”
“Safi, safi sana…acha tupige pesa ahahaha!” Steve aligeuza macho yake na kuyarejesha ulingoni ambako pambano lilianza kwa kasi ya aina yake.
Dame, jitu la misuli na uso wa hasira, aliruka ulingoni kama simba aliyejeruhiwa, akiingia kwa shambulio la kwanza. Alirusha ngumi nzito iliyopasuka hewani kama msumeno wa chuma.
Lakini Rocky alikuwa tayari. Alikwepa kwa ustadi, Aliruka na kutua kando akiepuka pigo la Dame kwa nyakati sahihi. Dame hakusita, aliongeza kasi, akimrushia mateke makali ya pembeni, lakini Rocky kwa haraka ya paka, alikwepa tena na kuachia teke moja matata likikosa shabaha na kuupiga ulingo kwa kishindo.
“Weeweeee!”
“Rockiiiiiiiii”
Sauti za wapambe hazikuwa mbali, zilisindikiza mtanange huu mkali.
Wakati Dame akiwa bado katika hali ya kujikusanya, Rocky alichukua nafasi hiyo. Akiwa na kasi ya umeme, aliruka mbele na kuachia ngumi ya kulia iliyolenga kwenye mbavu za Dame. Pigo hili lilisababisha sauti ya mgurumo toka kwa Dame. Dame alitikisika na kuyumba huku akijaribu kuleta ulinzi.
Rocky hakuacha, alirusha ngumi mbili nyingine moja kwa moja usoni mwa Dame. Ukali wa ngumi hizo ukamlazimisha Dame kurudi nyuma kwa hatua kadhaa.
Ulingoni, watu walishangilia kwa sauti za kishindo, wakihamasisha ujasiri wa Rocky. Franco na Kupa, machachari wa mtaa, walikuwa na macho ya ukakamavu, wakitazama kwa makini kila hatua ya pambano hili la kihistoria.
Dame akiwa na hasira kali, alirusha teke la juu lililolenga kichwa cha Rocky. Lakini kwa ustadi wa hali ya juu, Rocky alikwepa, alishuka chini na kuchuchumaa kisha akaruka juu na kupiga ngumi kali kwenye taya ya Dame. Ngumi hiyo ilitingisha kichwa cha Dame na tayari aliishiwa nguvu, hatimaye alianguka chini kama mti ulioangushwa na shoka.
Kengele ililia mara moja, ikitangaza mwisho wa pambano. Shangwe zililipuka, zikivunja ukimya wa usiku. Franco, akiwa na furaha ya ushindi wa mteja wake, aliruka juu ya ulingo, akishika mikono ya Rocky juu na kumtangaza kwa sauti kubwa,
“Na sasa tunamtangaza bingwa wa usiku huu naye ni Roooooocky!”
Shangwe zilirindima kwa Rocky, alitabasamu, akihema kwa nguvu, akipokea hongera kutoka kila upande. Lakini hakuweza kusahau machungu ya raundi ya kwanza, na akajua kuwa ushindi huu ulikuwa ni wa kwake tu.
Baada ya watu kuanza kutawanyika, Franco na Kupa walijikusanya pembeni, wakianza kugawa pesa zilizokusanywa kutoka kwenye kamari na machaguo ya mashabiki.
“Rocky, asilimia 40 yako hapa”
Franco alisema, akimpa kifurushi cha noti. “Asilimia 50 tunabaki nayo sisi, na Dame anapata asilimia 10.”
Rocky alichukua pesa hizo kwa unyonge, macho yake yakionyesha kutokuridhika.
“Haya si makubaliano yetu, tulikubaliana mshindi anachukua asilimia 60. Mambo gani haya? aliongea kwa maudhui huku sauti yake ikiwa na ukakasi.
“Hii ni biashara, Rocky. Hatuwezi kufanya kwa hasara.” Kupa alijibu kwa tabasamu la kejeli. “Unaweza kulalamika, lakini hii ndiyo sheria ya mtaa.”
Franco, alihisi hali inavyoweza kuchafuka muda wowote, aliingilia kati kwa sauti ya busara.
“Rocky, umeshinda bhana. Hii ni sehemu ya mchakato. Ushindi wako ni mwanzo wa safari ndefu. Nadhani ushaanza kuwa mteja wetu wa kudumu na jina lako limeanza kupaa. Tulia tufanye biashara”
Rocky alitazama kwa muda, akijaribu kuelewa kisha aliiamua kuachana na jambo hilo. Alikubali pesa hizo na kuondoka. Alijua kwamba huu ulikuwa mwanzo tu wa changamoto kubwa zaidi, na japo alihisi hakupewa stahiki yake, alikuwa tayari kwa chochote kitakachofuata. Shangwe zilianza kufifia huku mtaa ukirudi kwenye utulivu wa kawaida, lakini ndani ya Rocky, moto wa ujasiri na ari ulikuwa umewashwa kwa nguvu zaidi.
Mara baada ya kila mmoja kuondoka, Mwanamke mmoja aliyevaa kinyago cheusi usoni (Tesha)aliibuka karibu na maeneo ya ulingo. Alitikisa kichwa kwa udadisi na hali ya kuonyesha kuelewa jambo fulani. Alipiga hatua kadhaa huku akiwa makini kuona kama kuna mtu yeyote yuko pale na amemuona. Alipohakikisha kuwa hakuna aliyemuona aliondoka haraka sana eneo lile.
—------------------------------------------------------------
Jeshi la Polisi lilizingira eneoa la Gym ya Gacha Stone, hii iliashiria kuwa taarifa za mauaji zilishawafikia. Ulingo wote ulizungushiwa uzio wa uzi mwekundu, bado mwili wa Gacha ulikuwa chini ya ulingo na kamera ziliendelea kummulika. Inspekta Macha alionekana akiwa mwingi wa haraka, alitembea kwa hatua ndefu zilizomtafsiri kwa haraka kuwa alikuwa ni Afande mwenye umakini na uthubutu juu ya kazi yake. Pembeni yake aliongozana na madaktari wawili wa kiume waliovalia makoti meupe, licha ya yeye kuvaa kiraia lakini alikuwa maridadi mwenye mwili uliojengeka kwa mazoezi.
“Lolote?” Macha aliuliza kwa sauti kavu huku akitaka kujua mara baada ya yeye na wale madaktari kuingia ndani ya ulingo.
“Nothing (hakuna lolote). Angalia utajionea.” Sauti laini ya Afande wa kike ilimjibu. Ni Afande Asmin, alijibu akiwa na hasira kidogo huku akipepesa macho yake kando ya ulingo na Gym kote.
Macha alichutama, alidasisi mwili kwa umakini na kuona ngeu pamoja na michubuko mwilini. Pia alisoma kwa umakini lile neno la Champion, alitikisa kichwa na kumgeukia Asmin.
Asmin naye alitikisa kichwa kama ishara ya kuelewa ujumbe wa Macha.
“Nani alitoa taarifa?” Macha alimuhoji Asmin huku tayari wakiwa wanazunguka Gym ili kuona kama wangepata alama yoyote.
“Ni yule kijana” Asmin alinyoosha kidole chake upande wa kushoto ambako kulikuwa na kijana wa makamo ameketi kwenye kiti kwa huzuni.
“Ni nani yake?”
“Ni ndugu wa karibu na Gacha, tumeamua kumuacha kwanza ili apoze machungu na mahojiano tutafanya siku ya kesho.”
“Sawa na hakuna jingine? Kama kamera au kitu chochote cha maana?” Bado Macha aliendelea kuhoji, kwa hakika kesi hii ilikuwa ni ngumu na nzito kwao.
“Hakuna Afande. Tulikuwa tunakusubiri wewe ili uruhusu kutoa taarifa kwa umma pamoja na bodi ya ndondi.”
“Fanya hivyo Asunta…..”
“Naitwa Asmin na si Asunta, Afande.”
“Oohps! Samahani sana Afande Asmin.” Macha aliomba radhi kwa Asmin huku anaondoka. Asmin alirudi kwa maafande wengine na kuteta nao. Mmoja alitoa simu na kupiga mahala fulani huku wengine wakiubeba ule mwili na kuondoka nao.
Asmin alipiga hatua zake hadi kwa yule kijana, ndugu wa Gacha. Alijawa na huzuni huku machozi yakimtoka kimyakimya.
“Abdulal! Unaweza kuja kituoni kesho asubuhi?”
Asmin alimuuliza kwa huruma huku mkono wake mmoja akimpapasa kichwani kama ishara ya kumtuliza.
“N…nit..nitakuja” Abdulal sasa alishindwa kujizuia, alijikuta analia kama mtoto mbele ya Afande huyu ambaye ni Mwanadada wa makamo, aliyepanda hewani mithili ya twiga. Muonekano wake na kazi yake ilikuwa ni vitu viwili tofauti, alisatahilli kupanda kwenye majukwaa ya ulimbwende na uanamitindo.
“Pole sana, pole sana. Hii ni kazi ya mola haina makosa. Naelewa maumivu unayopitia.”
“Ndoto zangu zimekatika ghafla afande. Nitasimamiwa na nani? Nani ataniangalia? Naanzia wapi mimi?!”
“Pole, Pole sana. Afande Mseja?!” Asmin alipaza sauti kumuita moja ya askari walioko mule ndani.
“Naam Afande.”
“Ongozana na huyu dogo hadi kwangu, Asubuhi itakapofika ataripoti ofisini kwa Afande Macha kisha atarudi nyumbani kwaajili ya taratibu za mazishi.”
“Sawa Afande.”
Asmin aliinuka huku bado akimpa moyo Abdulal kwa kumbusu kwenye paji la uso kisha aliondoka.
Afande Mseja alimchukua na kuongozana naye ili kumpeleka kwa Afande Asmin.
—--------------------------------------------------------
Steve na Hakim walikwa na furaha kubwa, walicheza na kuimba huku wanahesabu fedha zao wakiwa kitandani.
“Aiseee! Hii ni nomaaa babuu! Hatujawahi ingiza thamani kubwa ya pesa kama leo.” Hakim alijimwaga kwa raha na furaha.
“Ujue najiuliza sana tulikuwa wapi? Mbona tulichelewa sana kufahamu lile chimbo la kwa Gogo? Ahaha! Ngapi hizo mwanangu?” Steve naye hakuwa nyuma, furaha ilidhihiri machoni na moyoni mwake.
“Oyaa! Laki Tisa na elfu hamsini na elfu tatuuuu” Hakim alimwaga pesa hewani kwa furaha. Hakika mioyo yao ilichanua mithili ya ua la asubuhi.
‘Ngo ngo ngo!’ Sauti kubwa ya kugongwa kwa mlango iliwashtua sana. Hakim alikusanya fedha zote haraka na kuziweka kwenye mkoba, Steve alijihami haraka na kuchukua gongo. Walitazamana kwa hofu huku kelele za kubishwa kwa mlango zikiendelea, Steve alifungua mlango kwa nguvu. looh! Kurupushani fupi ilizuka, Steve alimkosa Rocky kwa lile gongo.
“Steveee! Kwani vipi?” Rocky aligomba kwa nguvu, mikono yake myepesi ilizuia gongo la Steve.
“Oya! Acha utani bhana, unagongaje mlango pasi na kusema wewe nani! Dooh!” Steve alilalamika kwa afueni, alishusha pumzi ndefu na kuketi kwenye kiti.
“Kaka! Akili zilishahama tukasema leo tunaibiwa ahahaha!” Hakim naye alicheka baada ya kujua kuwa usalama ni wakutosha.
Rocky hakuzungumza, alijitupa kitandani akiwa hoi. Na sasa alianza kuyasikia maumivu yote aliyoyapata wakati anapambana na Dame.
“Vipi uko sawa? Au hawajakulipa wale jamaa ili tukawafanyizie?” Hakim aliuliza kwa shauku huku anamtazama Rocky pale kitandani.
“Wamelipa ingawaje wamekata kidogo na sio kama ambavyo tulikubaliana.”
“Achana nao,” Hakim alimtuliza. “Pale tunaweza kupiga pesa nyingi kwa muda mfupi. Kama tutakomaa basi mambo yetu yatakuwa sawa kwa uharaka.”
Rocky alikaa kimya akiwa amefunga macho yake, muda wote huo, Steve alitulia na simu yake akiperuzi kwa umakini taarifa anayoisoma.
“Oya wanangu!,” Steve aliwashtua kwa sauti yenye mashaka na mshangao. “Gacha Stone ameuwawa!”
Wote walikurupuka na kusogelea simu ya Steve. Alichokisema Steve ndicho ambacho kiliandikwa. Bodi ya michezo ya ndondi ilithibitisha kifo cha Gacha aliyeuwawa na mtu/watu wasiofahamika huku uchunguzi zaidi ukiendelea.
“Inawezekanaje kwa bingwa kama huyu kuuwawa?” Hakim alihoji kwa udadisi ingawaje kati yao hakukuwa na mwenye majibu thabiti.
“Aliyemuua si mtu wa mbali. Haiwezekani mtu wa mbali akamuua mwamba kama Gacha. Daah! Ngoja tusikilizie itakuwaje.” Steve alijibu kwa huzuni huku Rocky akitafakari kwa kina.
“Mmh! Itakuwa vigumu kujua kwa sasa, maana hata hii taarifa halijajitosheleza. Daah! Nilikuwa nampenda sana Gacha. Tuonane peponi mwamba”
Rocky naye alisikitika, Gacha alikuwa ni moja ya wanandondi anaowakubali na kuwafuatilia.
Chumba kilizizima kwa taarifa za kifo cha Gacha, watatu hawa wote walikuwa ni wapenda ndondi hivyo kwa namna moja au nyingine waliguswa na kifo hiki.
Baada ya kila mmoja kufunika macho yake kwa lengo la kutafuta usingizi, macho ya Rocky yalibubujika machozi taratibu na moyo wake ulijaa maombolezo juu ya kifo cha Gacha Stone. Hakuona raha ya usingizi, moyo ulimfukuta na machangu yalimjaa. “Brother, Brother, brother” Rocky alijisemea moyoni huku akifuta machozi yake. Ni wazi machungu haya si ya kishabiki tu bali lipo jambo jingine. Yamkini Siri ya mtungi ajuaye kata
Inaendelea……….

Comments
Post a Comment