Maangamizi: Hakuna Matata Gone Wrong. Sura ya 01, Agano liliosahaulika


 RIWAYA

Maangamizi: Hakuna Matata Gone Wrong 

Mwandishi: Haji Mgogoro

Mawasiliano: +255 784 382 101

hajimgogoro@gmail.com

Instagram & Facebook Haji Mgogoro

--------------------------------------



SURA YA 01.

Agano lililosahaulika 

                      (The forgotten covenant)


Zanzibar, Msitu wa Nuru - Karne za zamani.


Majira ya machweo yalitanda, jua likituma miale yake ya mwisho iliyokuwa ikichujwa na vichaka na miti mirefu ya kale. Msitu wa Nuru, mahali pa siri na heshima, palitetemeka kwa sauti za viumbe hai wa ajabu waliojificha kila kona kwa fumbo na hofu. Hewa ilikuwa nzito, harufu ya unyevu wa ardhi na majani yaliyooza iliijaza mapafu, huku sauti ya upepo wa mbali ikipiga mithili ya filimbi.

Miale ya jua ilipenya katikati ya miti mirefu, yenye mizizi mikongwe iliyoshonana kama mikono ya majitu, ilipenya na kutua kwenye eneo la wazi lililoonekana kutengwa kwa heshima ya nguvu kubwa isiyoeleweka. Sehemu hiyo ilikuwa maalum yenye kichwa kikubwa cha Simba mwenye macho yanayotoa miale ya moto.

Kichwa hicho hakikuwa cha kawaida, macho yake yaliwaka moto wenye uhai, yaking’aa kama makaa yaliyopulizwa, na mwanga huo uliokuwa ukimiminika ulionekana kuufanya msitu mzima kusimama kimya. Hata sauti za ndege zikaanza kufifia, kana kwamba hata viumbe wa msitu walitambua umuhimu wa uwepo huo.

Kichwa cha simba kilionekana kama mlinzi wa kale, aliyepewa jukumu la kulinda au kulaani. Ardhi ilizungukwa na alama za fumbo zilizoandikwa kwa michirizi ya mchanganyiko wa damu na majivu. Majani makavu yaliyoanguka kutoka kwenye miti ya juu yalikuwa yametanda eneo hilo, lakini hayakufunika ishara hizo za zamani.

Mbele ya kichwa cha simba kulikuwa na wazee watatu waliopiga magoti, waliobeba hekima ya vizazi na kijana mmoja mwenye uso wa uthabiti na macho yenye kuangaza matumaini aliyetangulizwa mbele kabisa ya simba. Wazee watatu wenye nywele ndefu na nyeupe zilizoshuka hadi mabegani mwao, walivaa nguo nyeupe tupu zilizowakilisha utakatifu wa desturi zao wakati yule kijana mwenye muonekano wa kishupavu (Jabari) alikuwa kifua wazi, amenyolewa kipara na kushikilia chetezo chenye kufuka moshi wa uvumba wenye harufu ya nguvu na usafi.

Hali ilikuwa ya ukimya wa heshima, isipokuwa sauti za lugha za mababu zilizotamkwa kwa sauti za chini na za kihekima na wazee wale. Mzee Jengo, kiongozi wa wazee (Mhina mkuu), alinyanyua mikono yake juu na kusema kwa sauti ya kutetemeka:

“Maafa yamekuwa makubwa, majanga yamekuwa makali, na watu wetu wanazidi kuangamia. Ni wakati wa kuamsha nguvu ya mababu zetu, Nguvu ya Urithi, iwe mlinzi wetu, iwe uponyaji wetu, iwe mwongozo wetu.”

Mzee Mwamba na Mzee Akili walilala kifudifudi na kunyoosha mikono yao mbele wakimuacha Mzee Jengo amepiga magoti huku Jabari bado amesimama.

“Eeeh Roho za Mababu, amka eeeh Roho za Zamani, sikiliza muito wetu eeh Sauti za Kale, eeeh Nguvu Tukufu! eeh Nguvu ya Urithi amka na utuponye”

Mzee Akili na mzee Mwamba waliendeleza Dua ya kuamsha Nguvu ya Urithi kwa sauti zilizofatana.


Jabari alipiga hatua mbili mbele kukabili kichwa cha simba akiwa mwenye shauku kubwa. Macho yake yalionekana kuwa na wasiwasi lakini moyo wake ulikuwa thabiti juu ya azma yake takatifu, alisema kwa sauti ya dhati.

“Eeh roho ya ardhi hii, enyi wazee nipo tayari sasa, nipeni nguvu ya kulinda watu wangu na….”

Lakini kabla hajaendelea, Mzee Jengo alisimama na kumshika begani kwa upole lakini kwa mamlaka.

“Subiri kijana wangu, acha papara ni lazima tambiko na dua hii imalizike na ndipo utakapokuwa Mhafidhina mkamilifu, kufanikisha hilo unatakiwa kukaa ukiyasema maneno ya mababu, hutakiwa kuacha hata litokee jambo lolote lile sawa?”

“Sawa, sawa eeeh Mhina wangu” Jabari alijibu kwa utii na kutulia.

Mzee Jengo alirudi nyuma na kupiga magoti tena. Jabari naye alirudi nyuma hatua mbili tena na kuongeza umakini juu ya tambiko.

“Roho ya ardhi hii, kwa viashiria vyote vinavyoupa ulimwengu uhai na viamke sasa. Ewe Bahari kuu, ewe Anga kuu, ewe Ardhi kuu, ewe Roho kuu, ewe Moto mkuu amka na ufunguke sasa….tunaiamsha nguvu kuu ya ulinzi na uponyaji, tuliyoachiwa na mababu zetu nasi tutaachia wajukuu zetu…..”

Sauti kuu za wazee watatu ziliungana kwa pamoja na kutamka maneno haya yenye nguvu na muashirio mkuu wa maamsho, maamsho ya Nguvu kuu, Nguvu ya Urithi.

Nje ya Msitu wa Nuru na kijijini (Fumba) anga likawa nyeusi ghafla, miungurumo ya radi ilisikia ikiashiria kuamka kwa Roho ya anga. Baharini nako bahari ikachafuka, kulipiga mawimbi makali pamoja na dhoruba ya upepo mkali kuashiria kuamka kwa Roho ya bahari kuu. Milimani nako volkano iliripuka, Roho ya moto mkuu ilisadiki maneno ya wazee.

Kadhalika upepo mkali ulivuma huku ukitoa sauti kali yenye kuogofya kuashiria kuamka kwa Roho kuu pamoja na roho ya upepo mkuu. Haya yote yalifanyika kwakuwa Roho ya Anga kuu ilisadiki kufanyika kwa hayo yote.

Katikati ya msitu napo upepo mkali uliendelea kuvuma, wazee wote waliamka na kupiga magoti na kufunga mikono yao. Upepo ulikatika ghafla na kiza kikali kikatanda, miale kutoka katika macho ya simba ilijikusanya na kutengeneza mfano wa tufe au duara la moto, moto uliotoa nuru kali amabayo ilishuhudiwa hadi na wanakijiji wa Fumba.

Hii ikawa ishara kwa wanakijiji wote, kila mmoja alimtoa mgonjwa wake ndani, mifugo yote ikatolewa mazizini, kila aina ya mmea na mbegu zilitolewa nje na watu wote wakawa nje ya nyumba zao kusubiri.

Nuru ya moto ikawa kali mara dufu, Jabari alianza kuhisi maumivu makali kutokana na miale kuwa mikali zaidi, 

“Usiende popote, endelea kuzungumza kwa ulimi wa mababu ni lazima jambo hili limalizike”

Mzee Jengo alimkumbusha Jabari, Jabari hakuwa na budi zaidi ya kuongeza uvumilivu.

Matone madogo madogo ya mvua yalianza kushuka taratibu, kadri yalivyo shuka ndivyo tufe lile la moto lilivyozimika na kubadilika.

Hatimaye mvua kubwa ikanyesha kwa dakika chache, kila mwenye ugonjwa alipona mara baada ya kuguswa na matone ya mvua, mifugo yote ikawa na afya tena, ardhi iliyokawa kame na kavu ilichanua na kupendeza, maua mazuri yalichanua na kufanya vipepeo na nyuki kurukaruka huku anga ikipedeza kwa ndege mbalimbali.

Mvua ilimalizika kunyesha licha ya kuwa wazee na Jabari hawakulowana na wala chetezo hakikuzimika bado kiliendelea kufuka moshi, tufe halikuwa la moto tena na badala yake liligeuka kuwa duara la bluu lenye kutoa cheche za rangi rangi za bluu, tufe hili halikuwa duara tu pia katikati yake kulikuwa na mfano wa jicho la simba lililoangaza kama nyota, lililoanzia juu hadi chini ya lile tufe.….na hii ndiyo Nguvu ya Urithi. Nguvu ya Kale, Nguvu ya Mababu na Mizimu.

“Alabin, Alaban alabin bonban.”

Kwa furaha kubwa wazee waliyasema maneno haya huku Nguvu ya Urithi ikiwa mikononi mwa Mzee Jengo.

Mzee Jengo aliweka lile tufe juu ya kichwa cha simba na kuongea maneno kwa lugha aliyoifahamu mwenyewe, lile jicho kwenye tufe lilifunguka na kuwamulika.

Mzee Jengo alitabasamu, tayari muamsho wa Nguvu ya Urithi ulishakamilika.

“Na sasa watu wetu wapo huru, shida zetu zote zimemalizwa na nguvu yetu tukufu,......eeeh Nguvu ya Urithi”

“.....Eeeeh Nguvu ya utulivu na amani” Mzee Akili na Mwamba walimalizia kwa kushukuru.


Mzee Jengo aligeuka na kuwatazama wote,

“Jabari, na huu ndio wakati wa kukufanya kuwa Mhafidhina mkamilifu, yaani mlinzi mkuu na kiongozi wa Nguvu ya Urithi. Ni wewe pekee ndiye utakayeweza kuiongoza nguvu hii.” aliweka kituo na kuendelea,

“Geuka shujaa wetu, geuka uipokee tunu hii inayowapata watu wachache waliochaguliwa na mababu zetu, watu wenye roho safi waliounganishwa moja kwa moja na roho za zamani, roho za kale roho za mizimu na mababu.”

Kabla Jabari hajageuka, Mzee Jengo aliingiza mkono wake kwenye chetezo na kuchukua kaa moja la moto, Jabari aligeuka na kumtazama Mzee Akili pamoja na Mzee Mwamba ambao walianzisha azimio la pili la tambiko lao, azimio linalokusidia kumtawadha Jabari kuwa Mhafidhina mkuu.

“Eeeh chemchem za hekima na ustahimilivu, eeh kivuli cha simba, eeh nyota ya kale, eeh sauti ya mababu mtazameni kijana wenu, mjukuu wenu mliyemteuwa kuwa Mhafidhina na sasa ni wakati wetu ili kumkabidhi kwenu.”

Mzee Jengo alimchoma Jabari kwa lile kaa la moto katika ya shingo lake kwa nyuma, Jabari alitoa machozi yaliyofuka moshi huku Mzee Mwamba na Mzee Akili wakiendelea,

“Obladi oblada ala bin bon ban.”

Mzee Jengo alitoka upande aliosimama na kujiunga na wazee wenzake, walitazamana kisha wote walitazamana na Jabari. Mzee Jengo alitikisa kichwa na kutamka kwa sauti yenye uthabiti.

“Jabari, kukamilisha azimio hili, yakupasa kuzunguka Nguvu ya Urithi mara mia moja, haupaswi kuacha wala kusita, unganisha nafsi yako na nasfi za mababu zetu….. obladi oblada ala bin bon ban.”

Jabari sasa aligeuka na kuanza mzunguko wake wa kwanza akiwa na chetezo mkononi.

Wazee walifunga macho yao na kuzama katika azimio hili huku nyoyo zao zikiwa na amani kwa kuchaguliwa kwake Jabari kuwa Mhafidhina Mkuu.

Kijijini hali ikiwa shwari, kilisikika kishindo kikubwa chenye kuogofya mno, kumbe ilikuwa ni chombo cha usafiri cha anga za mbali ama ndege kubwa ya chuma yenye umbo la uyoga iliyokita ardhini na kusabibisha mtetemeko. Wanakijiji wakiwa katika hali ya sintofahamu na kuulizana ni kitu gani kilichopo mbele yao, waliteremka viumbe wageni (Alien) kutoka anga za mbali kabisa, viumbe hawa walifanana na binadamu kiasi, lakini wao walikuwa na vichwa virefu, masikio marefu na sura zao zilitisha kiasi, ngozi zao zilkuwa za kijani na baadhi yao waliundwa kwa vyuma vitupu kuanzia kichwa hadi miguu.

“KIMBIENIIIIIII hadi kwenye Mti Mkuu harakaaa”

Sauti ya mlinzi ilisikika, sauti iliyoashiria kilichopo mbele yao ni hatari.

Taharuki ilizuka na watu walianza kukimbizana hovyo, kikosi cha walinzi waliovalia mavazi maalum walikuwa mbele ya wale wageni ili kukabiliana nao, mikono yao ilishikilia panga maalum zenye kumeta rangi nyekundu.

Wageni wale walitulia tuli pasi na kusema lolote, mlango wa ile ndege ulifunguka, walishuka maalien wawili wenye vyeo vikubwa, wakwanza aliitwa Ndenga, anayesifika kwa uhodari wa mapingano, wa pili wakike aliitwa Xyra (Zira) yeye alisifika kwa roho mbaya zaidi na ndipo aliposhuka jemedari Mkuu Xhozo (Shozo), kwanza yeye ndiye mbaya kuliko wote, alikuwa na macho manne, mawili makubwa kisha mawili madogo yaliyoambatana na pua pamoja na mdomo.

Macho yake yalizunguka kama lenzi ya kamera na kuyasoma mazingira yote.

“Nkosike sebhange o’mwana”

(hakikisha unampata yule mtoto)

Xhozo alimwelekeza Xyra na Ndenga kwa lugha yao kisha aliondoka pale, kuondoka kwake ilikuwa ni kama refa ameamuru pambano kuanza, walinzi walianza kushambuliana na maalien, Xrya aliruka angani na kutoweka eneo lile.

Jabari akiwa bado anaendelea na mzunguko wake, Xhozo aliwasili. Kwanza alianza kwa kuwacheka akiwa mita chache kuwafikia.

“Nyie binadamu wajinga, manadhani ulozi wenu wa zamani unaweza kutuzuia?”

“Vuruguuuuuuu!”

Mzee Jengo alifoka kwa kumwita jina ambalo walizoea kumwita.

“Tulifanya makosa makubwa sana kuifungua Njia ya Nyota, kisha tukawakaribisha na kuwafanya marafiki, nilijua tu ipo siku utakuwa haini, nilijua ipo siku utarudi kufanya ushenzi.”

“Hahahaha” Xhozo alicheka kwa sauti iliyojirudia,

“Jengo, leo umedhihirisha kuwa binadamu wote ni wapumbavu, hivi ulianzaje kuweka ushirika na sisi? Sisi tuna nguvu ya kila kitu na kwa hakika leo tutaitawala dunia yote kwa nguvu zetu, lakini pia……” Xhozo aliongea akiwa anawakaribia taratibu. “......kwa nguvu yenu, Nguvu ya Urithi”


Jabari alichukizwa na maneno ya Xhozo, alitaka kuacha mzunguko wake, lakini maneno ya Mzee Jengo yalimjia kichwani mwake ya kuwa anapaswa kumaliza mzunguko wote, kwa kujishinikiza hakuwa na budi kuendelea.

“Vurungu, nilikuondoa hapa, nilikuonya usirudi tena….ooh bado una tamaa ya kuipata Nguvu ya Urithi? Au ni wewe ulileta majanga ukijua kwamba ni lazima tutaiamsha nguvu ili uje kuichukua?” Mzee Jengo bado aliendelea kuzozana na Xhozo ama Vurugu kwa jina jingine.

“Ahahaha, eeh Mhina mkuu kuamsha kwenu Nguvu ya Urithi kumetufungulia tena milango kutoka nyumbani kwetu yaani kutoka Nyota ya Nne hadi hapa, lakini sijaja hapa kufanya mapatano, bali maangamizi na leo……”

Xhozo akiwa anajiandaa kushambulia, Mzee Akili aliinuka haraka na kumfuata, alijitahidi kupambana naye lakini hakuweza, Xhozo alitema moto na kumchoma Mzee Akili, Mzee Akili aliyeyushwa kama chuma ni mifupa pekee ilisalia. Loh! Hakika ni hatari.

“Jabari hakikisha unamaliza mzunguko wako, laa sivyo utalipa gharama kubwa”

Mzee Jengo alimsisitiza Jabari akiwa anainuka na Mzee Mwamba, wote sasa walimkabili vikali Xhozo.

Mpambano mkali ulizuka baina yao, Wazee walitumia ujuzi wao wa mapambano kumkabili kiumbe huyu kutoka nyota ya nne.

Xhozo alishindwa kufua dafu mbele ya Mzee Jengo na Mzee Mwamba, walimchapa kama mtoto na kumkalisha chini huku panga zao zilizopoa moto zikiwa shingoni kwa Xhozo.

“Hii ni nafasi yako ya mwisho Vurugu, ondoka na usirudi tena.” Mzee Jengo alitoa onyo la mwisho huku anahema kwa mpambano mkali.

“Sawa….sa-wa Jengo sawa, nitaondoka nawala sirudi tena.” Xhozo alijibu kwa majuto akihofia hatari ya kukatwa kichwa chake.

Jengo na Mwamba walitazamana na kumwachia Xhozo, hakika yalikuwa makosa makubwa sana. Vidole vya Xhozo viliota ncha kali za vyuma ambavyo viliishia katika vifua vyao wazee.

“Mzee Jengoooooooo!!”

Jabari alishindwa kuhimili kuona wazee wake wakidondoka chini huku damu zikiwatoka midomoni, aliruka juu kwa ustadi na kutua mbele ya Xhozo, hapo hapakuwa na mazungumzo ya mdomo, bali ya mikono mizito ya Xhozo na upanga mkali wa Jabari.

Shujaa huyu chipukizi hakufanya ajizi hata kidogo, hakutoa hata nafasi ya kupumua kwa Xhozo, aliachia mashambulizi mfululizo na kumuweka adui yake kwenye wakati mgumu. Licha ya Xhozo kutema moto wake lakini Jabari alijikinga kwa upanga wake wa miujiza, wakati upinzani mkali ukishika kasi, Mzee Jengo alifungua macho yake na kumtazama Mzee Akili ambaye alishafariki, taratibu alijivuta hadi mbele ya kichwa cha simba chenye Nguvu ya Urithi juu yake.

“Alabin alaban ala bin bon ban, eeeh Sauti za Zamani, najua ni makosa kuamsha na kuzimisha Nguvu hii kuu kwa wakati mmoja na gharama yake ni kubwa, hivyo basi kwa ulinzi zaidi ili nguvu hii isiingie mikononi mwa waovu, nipo tayari kulipa kwa Gharama Kuu. Jabari hawezi kushinda hii vita kwa siku ya leo, ni lazima nguvu hii ibaki mahali salama.”

Mzee Jengo alitoa kisu kidogo na kuchanja kiganja chake, kisha alidondosha damu juu ya Nguvu ya Urithi. Looh salaleee! radi kubwa ilipiga na kusababisha tetemeko kuu, tetemeko lililomtupa kando Xhozo na Jabari.

Kiza kikatanda ghafla, kilichosaidia ni ile nuru hafifu ya Nguvu ya Urithi, ilemetameta kwa mwanga wa wastani.

Mzee Jengo alisimam na kumgeukia Xhozo kwa hasira, “Vurunguu!! Leo ni mwisho wako, njia yenu itafungwa hivi punde na wala haitofunguka tena, na kama mtasalia duniani basi nguvu ijayo hivi punde itawaangamiza wote. Itakuwa mwisho wa hadithi yenu pamoja na dunia yenu.”

Mzee Jengo alimweleza Xhozo akiwa na uhakika wa kile anachokisema, kabla haijafanyika tafakuri yoyote, ghafla Nguvu ya Urithi ilisambaratika huku ikitoa chache zilizopaa angani, kichwa cha simba kilififia na kutoweka katika macho yao.

“Jengooo, huu si mwisho wetu. Hili ni Agano langu kwako na kijiji cha Fumba pamoja na huyu bwana mdogo. Hakika tutarudi tena na kuitwaa nguvu yenu ambayo ni kikwazo kwetu kufanikisha mambo yetu, eeh shujaa mdogo vita hii tutapigana tena mimi na wewe hakika leo hii ushindi ni wakwenu.”

Baada ya kusema haya, haraka sana Xhozo alitoka katika msitu wa Nuru na kurudi kule ambako ndege yao ilitua. Kijiji chote cha fumba kilikuwa kinawaka moto huku baadhi ya miili ya wanadamu na alien ikiwa imezagaa kwa chini.

“Vanu uti vanditukuta, nkelebete” 

(watu wote wamekimbia, wamekimbilia sehemu salama)

Ndenga alimjulisha Xhozo wakiwa kwenye uharaka wa kuondoka.

“Nsheva nge tempoo, vamoooos.” (hatuna muda tuondokeniii)

Xhozo aliwatahadharisha na haraka waliingia katika ndege yao huku Xyra akiwasili na mtoto mchanga mikononi mwake, Xhozo alitabasamu kisha hao waliondoka.


Jabari alimpakata Mzee Jengo katika mapaja yake, Mzee Jengo ambaye alikuwa hoi bin taabani.

“Jabari, mzunguko wako haukumalizika, wewe ndiye ulipaswa uwe Mhafidhina Mkuu, lakini kushindwa kwako…..”

“Mzee, sijashindwa Nguvu ya Urithi haipo mikononi mwa vurugu. Na juu ya mzungu wangu nadhani nimemaliza na kama sikumaliza basi ulibaki mzunguko mmoja tu.” Jabari alijibu kwa hofu huku akiwaza ni lupi litatokea kama mzunguko wake haukumalizika.


“Umeshindwa Jabari, umeshindwa…utapoteza nguvu zako zote za asili na utaishi kama wanadamu wengine, vita ijayo ni ngumu kuliko vita yoyote ile, ni vita itakayopiganwa katika nyakati za kisasa.” Mzee Jengo aliendelea kuongea kwa taabu, huku bado damu zinamtoka kifuani.

“Sasa itakuwaje? Ni wapi itapiganwa? Na nguvu iko wapi? Nani atawajibika kuilinda?” Jabari alijikuta anauliza maswali mfululizo,

Mzee Jengo hakujibu, badala yake alivua pete yake na kumvisha Jabari katika kidole chake cha mwisho.

“Kwa bahati mbaya, hatuna Mhafidhina mwingine hivyo yakupasa uishi hadi nyakati hizo za kisasa na uilinde Nguvu ya Urithi dhidi ya dola kubwa za kidunia hapo baadae. Vita zijazo ni mbaya zaidi na kali sana. Eeeh Njia ya Maarifa, eeh Sauti zenye Busara Eeeh Ulimwengu wa Maarifa, eeh Roho za Uhai mpokeeni huyu kijana muliyemchagua….Alabin Alaban Alabin bon ban”

Mzee Jengo alikata roho na kufariki mikononi mwa Jabari, Jabari alilia kwa sauti yenye ghamu na ghadhabu kuu lakini hakuweza kurudisha wakati nyuma, inampsa kusubiri huo wakati na kutekeleza jukumu lake kubwa, kuilinda Nguvu ya Urithi.


Usikose Sura ya 02.


Comments

Post a Comment