MWANDISHI: HAJI MGOGORO
WHATSAPP: +255784382101
CC: SIMULIZI EMPIRE
SURA YA 01
“Aagh!!! Mungu wangu, siamini jamani aaaaagh! Dianaaaa! yaaani……Maikoo! Maiko, Mume wangu na mdogo wangu toka nitoke? kwanini jamanii.” sauti ya Stella ilipasuka kwa uchungu, moyo wake ulijawa na simanzi alipoingia chumbani na kukuta picha isiyostahimilika.
Hakuamini kumkuta mume wake Maiko na mdogo wake Diana katika chumba chake na kitanda chake. Kitanda kilichokuwa chembe ya mapenzi yao sasa kilikuwa kielelezo cha usaliti.
Tukio hilo halikuhitaji ushahidi wowote kwani kalamu ilikutwa ikitiririsha wino taratibuu. Kwa hali ya sintofahamu iliyojitokeza Maiko alivuta bukta yake haraka huku Diana akijifunika na mashuka pale kitandani.
“Mke wangu naomba unisikilize, yaani ni……..” Maiko alijaribu kusema.
“Nyamaza Maiko, Usiongee chochote! Aagh! Haiwezekani. Yaaani siwezi tena kuvumilia ni lazima hizi taarifa baba ajue.”
Stella alifoka huku akiifunga vizuri bebeo yake iliyokuwa imebeba mtoto wa mwaka mmoja.
"Dada, tafadhali! Usifanye hivyo, nakuomba dada, itakuwa fedheha kubwa sana!” Diana alilia kwa dhati ya moyo, lakini maneno yake yalikuwa kama upepo kwa Stella. Bila kugeuka, Stella aliwapa kisogo, akafungua mlango na kuondoka huku machozi yakimtiririka kama mtoto.
"Shemeji, sasa itakuaje? Huu ni msala ujue, unadhani baba atafanya ninu akiskia hii taarifa?”
Diana aliuliza kwa sauti ya hofu, macho yake yakiwa hayatulii.
“Hakuna namna Diana, Dada yako hatakiwi kufika kwa Mzee.” Maiko alisema kwa msisitizo huku akivaa vesti yake nyeusi kwa haraka na kutoka kama umeme.
Stella alikuwa tayari barabarani, mwendo wake wa haraka ukizuiliwa na mtoto aliyembeba mgongoni. Alikuwa kama mnyama aliyejeruhiwa, akitembea bila kujua mwelekeo, akili yake ikiwa imevurugwa kabisa.
“Ooh! Kwahiyo mimi hukujali kitanikuta nini si ndiyo? Niachie niondoke maiko, hebu niachie bwana….” Stella alifoka huku akijitahidi kujinasua, lakini Maiko alishikilia kwa nguvu.
“Mke wangu ee, naomba unielewe basi ni shetani tu, mke wangu tafadhali Sana.” Maiko alisema kwa sauti ya unyenyekevu.
“Maiko hunielewi eeeh? Sitaki nasema! Niachie mkono unaniumiza, upuuzi wenu msimlaumu shetani.” Stella alipandisha sauti, hasira ikiwaka kama moto.
Wakati vuta n’kuvute hiyo ikiendelea, Diana alifika akiwa na kigauni kifupi cha mabega wazi, fadhaa ikitawala usoni kwake.
Maiko alimkunja vema Stella hata akamtoa mtoto mgongoni na kumpatia Diana.
“Huendi kokote Stella utanisamehe tu.” Maiko alimbeba Stella kwa nguvu na kurudi nae ndani, licha ya matusi mazito aliyopata kutoka kwa mkewe huyo wa ndoa kwa miaka mitatu.
Ndani kulitawala ukimya takribani robo saa, Hakuna hata aliyejaribu kuzungumza. Hali ambayo haikuzoeleka kabisa katika nyumba ya Maiko, kijana wa miaka 27 anayeendesha maisha yake kwa kuuza mbogamboga na matunda kwa bei ya jumla.
“Dada nakuomba shusha jazba, bora tuongee yaishe humu ndani.” Diana aliomba kwa unyenyekevu.
“Nini? Dada au mke mwenza? Niwe dada yako na mume tushee? Maiko kufunga mlango hakunizuii sawa? Niue basi ili nisiseme kokote.” Stella bado alibwata vikali.
“Stella mke wangu…….” Maiko alishindwa kuendelea baada ya mtoto kuanza kulia, Stella alimpokonya Diana Mtoto, na kuishia zake chumbani.
“Hii imekua ijumaa ya moto sana, hebu kavae nguo Basi.” Diana aliingia chumbani kwake baada ya shemeji yake kutaka hivyo.
“Stella amechacha leo, Sijui itakuaje!?” Maiko alitafakari afanyenini kumtuliza mkewe, hakika ilikuwa ni siku ngumu kwake.
—---------
Jioni hiyo, Stella alijitayarisha kuondoka. Mabegi mawili makubwa yaliketi mlangoni, tayari kwa safari isiyojulikana. Maiko aliingia, alimkuta Stella akifunga begi lake la mwisho.
“Sasa unaenda wapi na hayo mabegi yote?” Aliuliza Maiko kwa mshangao wa makusudi, lakini Stella hakujibu lolote.
“Stella mke wangu! Utaleta balaa ujue, wazee wako kama unavyojua presha zao ziko juujuu. Hebu tafakari kabla hatujajutia zaidi, nakuomba Basi mke wangu. Nadhani unajua kuwa Mama yako hawezi kustahimili hili jambo.” Maiko aliongea kwa sauti ya unyenyekevu, akijaribu kumshawishi mke wake.
Stella aliyatafakari maneno ya Maiko, hasa lile suala la presha hususani kwa mama yake, Bi.Rita. Stella aliishia kukaa kitandani machozi yakimtoka.
“Najua unaumia sana, lakini……..”
“Hebu nyamaza basi nawewe.” Stella alimkatisha Maiko kwa haraka. “Npishe nahitaji kuwa mwemyewe, unaelewa? Ondokaaa!!”
Maiko aliondoka zake baada ya kuona mkewe kapandisha hasira zaidi. Licha ya Ijumaa hiyo kuwa yenye kasheshe kwa Maiko, lakini kwingineko nako hali si shwari.
“Jamani yaani familia nyengine shida tupu, ukiolewa tu, basi jua umeolewa na familia nzima.” Khadija alifoka vikali baada ya Mama mkwe wake kuingia ndani. “Hivi we mama usokaa kwenu ukatulia kitu gani? Mume wangu mmemgeuza mungu wenu sio? hata mkiumwa na mbu basi yoyoyoyo!! mmekuja. Yaani mnakera, hamjui tu.” Khadija alibetua midomo kwa dharau na kuketi kwenye sofa huku akimtazama mkwewe ambaye alikuwa amesimama mlangoni.
“Khadija! Maneno gani hayo kwa mkweo jamani? Au hujafunzwa kwenu?” Kwa mshangao, rafiki wa Khadija, Fetma alimuuliza.
“We hujui tu Fetma, wanakera hawa hadi keroo.” Bado Khadija alijibu kwa dharau.
“Khadija bwana, staha Basi hee!” Fetma alimkaripia Khadija kisha aligeuka kutazama mlangoni.
“Mama karibu mbona waishia mlangoni?” alijaribu kutuliza mawimbi.
“Wenye nyumba hawajanipokea, si bora tu niondoke zangu!” Bi Siwajibu alilalamika kwa uchungu, akimwangalia Khadija kwa macho ya hasira. “Ila akija mumeo, mwambie kuwa pesa za mirathi ya baba yake zimetoka, aje nyumbani jioni.” Aliongeza kwa sauti nzito, kisha akashika kitasa na kufungua mlango kwa nguvu.
“Aah! Bi Siwajibu! Hata maji hunywi? au ni kweli unagubu kama mkweo anavyosemaga?” Fetma aliongea kwa utani kwa kwakua yeye na Bi Siwajibu ni watu wa kabila moja na aliyajua hayo toka kwa rafiki yake wa damu Khadija.
Bi Siwajibu hakujibu, liondoka zake kwakuwa ujumbe wake ulishafika.
“Mmmh shost! Siku nyingine utapishana na gari ya mshahara bureee, umeona Sasa.” Fetma aliongea kwa kicheko hafifu huku akiyatupa macho yake kwa Khadija.
“Achana nae, ukute wala hizo pesa hakuna. Hawa wakwe waswahili hii ndo dawa yao, wanapenda sana kuingilia ndoa za watoto wao, lakini kwa Khadija wamechemka.”
Kwa kujinata Khadija aliyasema, na hii haikuwa ngeni kwa Fetma. Mara kadhaa ameshuhudia Khadija akigombana vikali na ndugu wa mumewe pamoja na mkwewe.
“Hii tabia nakuonyaga sana besti, utakuja kulia siku moja, shaurilo!” Fetma alionya kwa sauti kubwa, huku akitabasamu.
“Fetmaaa! Jafari hapa kafika bwana na hachomoki ng'o, hajaniacha jana wala juzi sembuse leo?” Khadija alisema kwa majigambo, akiamini kuwa kila kitu kilikuwa chini yake.
“Hujui ivo, huenda kesho.” Wote waliangusha vicheko na Fetma aliaga kuelekea kwake.
—--------------------------
Majira ya saa mbili usiku, ukimya ulikuwa umetawala ndani ya nyumba ya Stella, lakini hisia za machafuko zilikuwa dhahiri. Stella aliingia jikoni kwa hatua za haraka, uso wake ukionyesha machungu ya siku nzima. Alifungua kabati na kuchukua sufuria, akijiandaa kupika chakula cha usiku. Kabla hajaanza, sauti ya mdogo wake ilikatisha mawazo yake.
“Dada, we pumzika tu. Acha nipike.” Diana alisema kwa sauti ya kujikomba, akijaribu kuonyesha huruma.
Stella aligeuka ghafla, macho yake yakiwa makali kama upanga uliosuguliwa. “Usilete drama zako hapa!” alifoka, sauti yake ikijaa uchungu na ghadhabu. “Kumbe kila nilipopumzika, wewe ulifanya kazi ya kujirusha na mume wangu? Malaya mkubwa wewe, tena, usiniite dada yako, sawa?”
Maneno hayo yalikuwa kama risasi zilizotolewa kwa hasira, zikitua moja kwa moja moyoni mwa mdogo wake. Diana alitetemeka, macho yake yakiwa na mchanganyiko wa hofu na aibu, lakini hakusema neno.
Stella hakusubiri jibu. Alitoka jikoni kwa haraka, akaelekea sebuleni ambako mtoto wake alikuwa amelala kwenye sofa. Alimbeba mtoto kwa upendo lakini macho yake yalikuwa na huzuni iliyofichika. Hakuhitaji kuuliza; alijua Maiko, mume wake, hakuwa ndani.
Alitoka nje, akivuta pumzi ya hewa safi ya usiku huku mawazo mazito yakimkaba. “Huu ndio mwisho.” alijisemea kimoyomoyo, macho yake yakitazama mbali kana kwamba yalikuwa yakitafuta suluhisho kwenye giza la usiku.
—--------------------
Mwendo wa kutoka Tandika hadi Majengo, haukuwa mrefu, lakini kwa Stella, kila hatua ilionekana ndefu kutokana na mzigo wa mawazo aliosheheni kichwani mwake. Alipofika mbele ya geti la nyumba ya Mzee Ntema, alibisha hodi kwa nguvu, sauti yake ikisikika wazi kupitia kimya cha usiku.
Mlinzi alifungua lango, na bila kusubiri maelezo zaidi, Stella aliingia moja kwa moja ndani ya nyumba.
Kabla hata hajapata nafasi ya kusalimia, kibao kizito kilitua kwenye shavu lake, kikitoka moja kwa moja mkononi mwa Mzee Ntema.
Stella alisimama kwa mshangao, akijishika shavu huku macho yake yakiwa na mchanganyiko wa uchungu na mshangao. Alipotazama kwa umakini, macho yake yakakutana na Maiko aliyekuwa ameketi kwenye sofa. Uso wa Maiko haukuwa na hisia zozote, alisalia kimya kana kwamba hakuwahi kuwa sehemu ya tukio lolote lenye utata.
“Baba! Kulikoni? Mbona kama hivi?” Stella aliuliza kwa sauti ya kutoelewa huku kigeuka kila upande wa sebule. Aliweza kusoma wazi hasira zilizojaa katika nyuso za kila mmoja, huku Maiko akiwa mkavu na kimya.
Mzee Ntema alifoka kwa sauti nzito, “Stella, nirudishie binti yangu hapa nyumbani! Mwanangu mimi si kahaba wala muhuni kiasi cha kuja kupakwa hayo machafu yako!”
“Mama, kunani? Mbona sioni kinachoeleweka hapa?” Stella alisema huku akimtazama Maiko, akitegemea kupata majibu kutoka kwa mume wake. Lakini Maiko alionekana kuepuka macho yake, kichwa chake kikiwa kimeinamishwa kwa aibu au kujisalimisha kwa hali fulani.
Mzee Ntema aliendelea kwa sauti ya kukemea, “Stella, Diana amekuwa kwako tangu ukiwa mjamzito hadi umejifungua. Lakini shukrani yako kwake ni kumfedhehesha na kumchafulia jina mbele ya kila mtu?”
Stella alikata kauli ya baba yake kwa ghadhabu, “Baba, subiri kwanza. Maiko, umewaambia nini hawa wazee? Nakuuliza umewaambia nini? Au umewaambia kuwa nimekufumania na Diana chumbani kwangu? Mwanaume mchafu wewe!”
Kauli ya Stella ilizidisha moto sebuleni hapo. Bi Rita, mama wa Diana, aliinuka ghafla, sauti yake ikijaa hasira kali. “Stellaaa! Usitake nitapike nyongo hapa! Ndio maana nikasema mlete mwanangu hajanishinda kumlea sawa.” Bi Rita alifoka mithili ya mbwa kichaa baada ya kauli za Stella kubugudhi ngoma za maskio yake.
“Hivi huoni aibu? Maneno yako ni matusi ya wazi mbele yetu! Uhuni wako fanyia huko na mume wako, sio hapa kwangu!” Ntema aliachilia ulimi wa moto kwa stella, stella ambaye hakujua chanzo cha yale yote.
Stella alibaki ameduwaa, hajui wapi pa kuanzia au pa kuelekea. Kila mtu aliyekuwa pale alionekana kumhukumu, na hata Maiko, ambaye alipaswa kuwa upande wake, hakuwa tayari kusema lolote kumtetea.
—--------------------------

Comments
Post a Comment